Miradi ya wizara ya ardhi inavyochochea umaskini Tanzania.

Na Chrizant Kibogoyo

KUTOKANA na wabunge, madiwani na wenyeviti wa vijiji na mitaa kushindwa kutumia sheria nzuri zilzizopo kulinda maslahi ya wananchi katika ardhi, Watanzania wanatakiwa kufuata nyayo za hayati Mwalimu Nyerere aliyetangaza hadharani kumuunga mkono na kisha kumpigia kura mgombe wa NCCR Ndg Paul Ndobo kwa ajili ya Ubunge wa Jimbo la Musoma Vijijini mwaka 1995 na kumuacha mgombea wa CCM aliyekuwa na tuhuma za kufilisi ushirika.

Ikiwa hayati Mwalimu Nyerere muasisi wa TANU na baadaye CCM aliweza kutambua umuhimu wa kuweka maslahi ya nchi mbele kabla ya maslahi ya chama chake cha CCM kwa kuchagua kiongozi bora na sio bora kiongozi kwa kuwa katoka CCM. Mwaka 2009 na 2010 Watanzania wanatakiwa kuamka na kutumia vyema haki zetu za kikatiba kuchagua timu ya viongozi ambao watakwenda kuweka maslahi ya taifa mbele na sio maslahi ya vyama na binafsi Bungeni.

Sheria ya Ardhi namba 4 ya 1999 imeanda utaratibu muafaka na shirikishi kweli kweli wa kuingiza eneo katika MPANGO WA URASIMISHAJI MASLAHI YA WANANCHI KATIKA ARDHI. Ni kutokana na umakini wa sheria hii ndio maana watendaji wa Wizara ya Ardhi, Halmashauri za Wilaya na Miji wanaikwepa kwa kuwa hawatapata chochote na kupendelea kuwapoka wananchi ardhi zao kienyeji tu.

Hivyo suala la urasimishaji ardhi za wananchi ni lazima wananchi walifanye kuwa ajenda ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka huu na uchaguzi mkuu wa mwakani kwa kuwauliza wagombea wanaotaka kurudi ni kwanini walishindwa kutumia sheira hii kurasimisha maslahi ya wananchi katika ardhi?

Ni kwanini walikaa kimya wakati Watendaji wa Wizara ya Ardhi, halmashauri za Miji na Wilaya walipokuwa wakikiuka Sheria za ardhi na kanuni za ulipaji fidia?

Sambamba na hilo ni lazima wananchi wawahoji viongozi wanaotaka kurudi ni kwanini walishindwa kusimamia utekelezaji ?

Ufuatao ni uzoefu wangu katika kushughulika na masuala ya fidia za ardhi kwa takribani miaka miwili. Mara tu baada ya wakazi 259 wa eneo la Luguruni kulipwa fidia tarehe 18 na 19 Desemba 2007, walilazimika kuacha shughuli zao za uzalishaji mali na kutumia kipindi cha miezi tisa hadi Septemba 2008 kutafuta haki ya kulipwa fidia kwa mujibu wa bei ya soko kama inavyoelekezwa na Sheria ya Ardhi namba 4 ya mwaka 1999 kwa kuendesha mikutano, kutafuta elimu ya sheria za ardhi, kukwaruzana na maafisa wa wizara na wapima ardhi, kufanya maandamano n.k.

Kwa nchi ambayo bado iko nyuma kimaendeleo hii ni dosari kubwa. Na baada ya kudhihirika kuwa wapo watendaji waliosababisha hali hiyo na Serikali kulazimika kuwaongezea wananchi fidia walistahili kuchukuliwa hatua za kinidhamu ili liwe fundisho kwa watendaji wengine wa aina hiyo.

Lakini , hadi sasa watendaji bado wanatamba katika nyadhifa zao wakiendelea kuwakorofisha wananchi katika maeneo mengine na hivyo kuwalazimisha kuacha shughuli za uzalishaji mali ili kudai haki zao za kisheria.
Mhe John Chiligati mara tu baada ya kuteuliwa kushika wadhifa wa waziri katika Wizara ya Ardhi, alilazimika kutembelea eneo la Luguruni, Kibamba tarehe 15 Machi 2008 kutatua mgogoro huo.

Kufuatia kushuhudia mwenyewe ukiukwaji mkubwa wa sheria, kanuni na taratibu alilazimika kuwaondoa kwenye mradi wathamini mali waliofanya uthamini wa mali za wakazi wa Luguruni kwa kutumia madaftari badala ya nyaraka halali za Serikali zijulikanazo kama VAL FORM 1 na 2 na kuleta timu mpya iliyoongozwa na ndg Mulokozi. Timu mpya ilifanya kazi nzuri ya kuwashirikisha kikamilifu waathrika 259 katika uthamini wa pili uliofanyika kati ya Mei na Agosti 2008. Wafidiwa walipatiwa haki ya kuorodhesha mali zao kwa usahihi katika form ijulikanayo kama VAL FORM Namba 1; wafidiwa walipatiwa fursa ya kutosha kuhakiki idadi na usahihi wa orodha ya mali zao kabla ya kuweka sahihi mbele ya kiongozi wa Mtaa na mthamini mali.

Hivyo kila msomaji wa makala hii, atakayehusika katika zoezi la kufanyiwa uthamini anatakiwa kudai haki ya kuorodhesha mali zake katika katika fomu hiyo kwa usahihi na akiridhika ndipo aweke sahihi yake mbele ya kiongozi wa eneo lake na si vinginevyo.
Kwa uzoefu wangu wathamini mali wengi hujifanya kuwa wana haraka kwa nia ya kumchanganya mwanachi.

Kila mara mwanachi anapaswa kukumbuka kuwa ardhi aliyonayoishikilia ina thamani kubwa na taasisi iliyomtuma mthamini mali ndio inataka ardhi hiyo hivyo masuala ya haraka hayapo kabisa.

Kwa mradi wa Luguruni katika uthamini mali wa awali, Wizara ya Ardhi ilikuwa imewalipa waathirika wa Luguruni kwa kiwango cha Shs 300 kwa Mita 1 ya Mraba ilihali tokea mwaka 2005 bei halisi ya viwanja katika eneo la Kibamba ilikuwa ni kati Shs Milioni 4 hadi 6 kwa kiwanja cha Mita 20 X 20 chenye Mita Mraba (20 X 20= 400); sawa na Shs 10,000/= hadi 15,000/= kwa Mita 1 Mraba ( 6,000,000/= ÷ 400 Mita Mraba= 15,000/=). Hivyo Wizara ya Ardhi ililipa fidia kwa kiwango cha kati ya 2-3% ya bei halisi ya ardhi eneo la Kibamba.

Kazi nzuri ya uthamini iliyofanywa na timu mpya ilingia dosari pale Waziri Chiligati aliposhindwa kutimiza ahadi yake aliyoitoa tarehe 25 Mei 2008 katika ukumbi wa Urafiki alipokutana na waathrika hao na kuahidi kuwa mara tu baada ya wizara yake kukamilisha utafiti mpya wa bei za soko la ardhi na nyumba katika eneo la Kibamba ataitisha mkutano mwingine wa kujadili viwango vipya vitakavyotumika katika kuwalipa fidia. Badala yake Wizara ya Ardhi ilijiamulia kutumia kiwango kipya cha Shs 1,977/= kwa Mita 1 Mraba sawa na Shs 1,977 X Mita Mraba 400=Shs 790,800/= kwa kiwanja cha Mita 20 X 20.

Kutokana na Waziri Chligati kushindwa kutimiza ahadi yake ya kuhakikisha wizara yake inafanya majadiliano na waathirika kuhusu viwango vitakavyotumika katika kuwalipa fidia.
Yeye binafsi na watendaji wa wizara yake walivunja Sheria ya Ardhi namba 4 ya mwaka 1999 kifungu 3(1)f cha kinachosisitiza “kufanyika kwa mapatano pale maslahi ya ardhi waliyo nayo wananchi yanapoathriwa kwa namna yoyote ile”.

Kutokana na kuvunjwa kwa kifungu hicho wizara ya Ardhi ilifanikiwa kuwalipa waathirika wa Luguruni 13% tu ya bei halisi ya ardhi katika eneo la Kibamba.

Na hivyo fidia hiyo kutoweza kukidhi haja ya waathirika kujipatia viwanja mbadala vyenye hadhi kama ambavyo walikuwa navyo yaani kufikika kirahisi, kuwa jirani na huduma za kijamii kama vile umeme, maji, usafiri, shule, maduka, ajira n.k Upo ushahidi wa kimaandishi unaonyesha kuwa wengi wa waathrika wa Luguruni walilazimika kuchota fedha zaidi kutoka katika fedha walizofidiwa nyumba zao ili kumudu kununua viwanja mbadala kwa bei za soko za kati ya Shs Milioni 4 hadi 18. Huu ulikuwa ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, haki za makazi na haki zinginezo za waathrika hao 259.
Kutokana na ushirikishwaji kukosekana kabisa Wizara ya Ardhi ikajiamulia kupandisha kiwango cha fidia za nyumba kutoka kati ya Shs 100,000/= na 150.000/= hadi 250,000/= na 300,000/= kwa Mita 1 Mraba ya nyumba.

Kwa mujibu wa wakandarasi wa majengo, ili mwananchi aweze kujenga nyumba na kuikamilisha ikiwa na huduma zote muhimu ikiwemo umeme, maji, barabara n.k. kama zilivyokuwa nyumba nyingi zilizobolewa eneo la Luguruni atahitaji kiasi cha ya Shs 500,000/= hadi 650,000/= kwa Mita 1 Mraba kulingana na hadhi ya jengo husika.

Hivyo kutokana na waaathirika wa Luguruni kutoshirikishwa katika utafiti wa bei za soko walipunjwa kati ya Shs 250.000/= hadi 400,000/= kwa Mita 1 Mraba ya jengo.

Tukikumbuka kuwa pia waathrika hawa walilazimika kuchota fidia za nyumba ili kumudu kujipatia viwanja mbadala kwa ajili ya ujenzi wa nyumba mpya, ni wazi kuwa wengi walishindwa kujirejeshea viwango vya makazi kama waliyo kuwa nayo hapo awali.

Sheria, kanuni na taratibu za fidia zinaelekeza ufanyike utafiti wa bei za soko katika eneo husika kabla ya zoezi la uthamini mali kuanza.

Kwa kuwa haiwezekani mtu kutoka mbali akamzidi mwejnyeji ktika kufahamu bei za ardhi, vifaa vya ujenzi na mazingira ya ujenzi katika eneo husika, ni muhimu wananchi wakadai kushirikishwa katika utafiti huo na kufanya majadiliano kuhusu viwango vitakavyotumika kuwalipa fidia ndipo wakubali kuingia katika zoezi la uthamini mali.

Kukubali kuingia kwenye zoezi la uthamini mali kabala ya viwango vya malipo havijatangazwa hadharani ni kosa lililowagharimu waathrika wa Luguruni kwa kukosa ufahamu.

Habari kwa hisani ya
Chrizant Kibogoyo, ambaye ni mwanaharakati wa masuala ya ardhi.
Anapatikana kwa simu 0787-125599 /0719-126575.

Comments

Popular posts from this blog

FAMILIA YANGU ILIPOTEMBELEA KIJIJI CHA WATOTO YATIMA CHA FURAHA MBWENI KINACHOSIMAMIWA NA MASISTA WA KATOLIKI WA SHIRIKA LA KIMISIONARI LA BIKIRA MARIA MAMA WA YATIMA SIKU YA JUMAPILI TAREHE 17 JANUARI 2016

Rest In Peace Son of Africa, Meles Zenawi.