hata mimi nimeipenda hii makala.
MAKALA NILIYOIPENDA WIKI HII:Utatu usio mtakatifu: Siasa, dini na biashara
KUNA namna mbili kwa mtu kusafisha chumba chake; unaweza kufagia chumba, ukazoa takataka na kuzitupa. Lakini waweza pia kuzifagilia takataka chini ya jamvi.
Ukifanya hilo la mwisho bado atakayeingia chumbani kwako ataona chumba kimesafishwa. Huko ni kujidanganya kwa mwenye chumba. Akiendelea na tabia hiyo, iko siku uchafu ule utaanza kuvunda na kunuka. Asipoinua jamvi kuondoa uchafu unaovunda iko siku ataambiwa na wengine; kuwa chumba chako kinanuka.
Katika nchi yetu tumeanza kuona dalili za siasa kuchanganyika na dini na biashara. Huu ni utatu usio mtakatifu. Hapa kuna tatizo. Kuna takataka tunazozifagilia chini ya jamvi, kisha tunaimba; nchi yetu ni ya amani na utulivu. Kwamba nchi yetu ni safi kabisa.
Kufanya hivyo si kuitendea haki nchi yetu tuliyozaliwa. Tatizo tunaliona. Ni wajibu wetu wa kizalendo kuzungumza kinagaubaga, kuwa hapa kuna tatizo. Maana Watanzania sisi tuna hulka ya ajabu kidogo. Wakati mwingine tunaamini kuwa kama jambo unalinyamazia, basi halipo hata kama lipo. Tatizo unaliona, lakini unachofanya ni kunyamaza kimya tu. Kinachofanyika hapa ni kufagilia tatizo chini ya jamvi badala ya kufanya jitihada ya kuliondoa.
Kwa mtazamo wangu, kuna tatizo kubwa katika uongozi wetu wa kisiasa. Tumeruhusu siasa kuingiliwa na dini na biashara kwa maana ya baadhi ya wafanyabiashara hata viongozi wa kidini wanaitumia siasa katika kufanikisha malengo yao. Kinachotokea sasa pia ni hata kwa baadhi ya wanasiasa kuitumia dini na wafanyabiashara kufanikisha malengo yao.
Kuna hali ya ” kuna mgongo wangu niukune wa kwako”. Mfanyabiashara anatoa ufadhili wake katika siasa ili baadaye siasa imsaidie katika biashara yake. Kiongozi wa taasisi ya kidini anaipigia debe siasa kwenye nyumba ya ibada ili siasa nayo imsaidie katika kujijenga. Hapa tuna viongozi wa taasisi za kidini waliojiingiza katika biashara na siasa. Bado tuna misamaha ya kodi kwa vinavyoingizwa nchini na taasisi za kidini. Wakati mwingine misamaha hii kimsingi ni kwa taasisi za kidini zinazofanya biashara. Naam. Hata kwenye baadhi ya taasisi za kidini kuna uozo na ufisadi uliokubuhu.
Hakuna dhambi kwa kiongozi wa kidini au mfanyabiashara kujihusisha na siasa, lakini, katika ubia huu wa siasa, dini na biashara hakuna utaratibu uliowekwa ili ufuatwe kwa minajili ya kuepuka mikanganyiko itakayowakanganya na kuwaathiri Watanzania wanyonge walio wengi. Ndiyo maana, katika makala iliyopita, nilizungumzia umuhimu wa jambo hili kuwekwa katika Katiba.
Ni vema na busara kabisa tukawa na taratibu na nidhamu ya kuzifuata taratibu. Na nidhamu ya kufuata taratibu inatokana na sheria na adhabu zinazoendana na kukiukwa kwa taratibu hizo.
Na hapa mpira uko ndani ya chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM). CCM ni chama tawala, hivyo kina wajibu wa kwanza wa kuandaa taratibu zitakazofuatwa ndani ya chama hicho inapohusiana na uongozi wa kisiasa. CCM hakipaswi kuwa ni chama kinachopambana ili kiishi. Tayari kiko madarakani, hiki si chama cha upinzani.
Ndani ya CCM imeanza kubomoka misingi iliyokianzisha, kuanzia vyama mama vya TANU na Afro- Shiraz. Hili ni jambo la hatari sana. Ikumbukwe, vyama mama kwa CCM, TANU na Afro- Shiraz, vilikuwa ni kimbilio la makabwela, kimbilio la wanyonge.
Lakini, CCM ya sasa inakimbiliwa na wafanyabiashara, wasomi na wajanja wengine. Wasomi hapa kwa maana ya hata wale wenye taaluma zao, wako tayari kuzikimbia taaluma zao na kuingia kwenye siasa za vyama, hususan CCM. Baadhi yao wanasukumwa huko kwa ajili ya kutafuta maslahi zaidi. Maslahi binafsi. Na kuna wanaoambiwa; ”Mkitaka mambo yenu yawanyokee, njooni CCM”. Si mambo ya wananchi, ni mambo yao binafsi!
CCM ya sasa inakimbiliwa hata na baadhi ya viongozi wa taasisi za kidini. CCM ya sasa ni taasisi kubwa. Ndani yake ina watu wa kila namna. Kuna makundi. Kuna majungu na fitna. Kuna kupakaziana, kuchafuana na kusafishana.
Naam. Kuna wanaokimbilia ndani ya CCM kwa kuamini katika malengo na madhubuni ya kuanzishwa kwa chama hicho. Lakini kuna wanaokimbilia ndani ya CCM wakiwa na malengo na madhumuni ya kwao binafsi yasiohusiana kabisa na ya CCM. Kwao wao, CCM ni sawa na daraja la miti la kuwasaidia kuvuka na kufika wanakotaka kwenda.
Baadhi wako tayari kutumia mamilioni ya shilingi kukimbilia uongozi ndani ya chama hicho. Wanakimbilia ndani ya chama kujificha, kuficha maovu yao, kulinda na kutetea maslahi yao binafsi na ya makundi yao.
CCM ina nafasi ya kujisahihisha na kuuvunja utatu huu usio mtakatifu. Si udhaifu kwa kiongozi au wanachama wa chama cha siasa kukiri udhaifu na kujisahihisha. Mwalimu Julius Nyerere katika kijitabu chake cha ” Tujisahihishe” anaandika; ”Nataka kutaja makosa machache ambayo mara nyingi huzuia Umoja wowote kuwa imara hata ushindwe kutimiza madhumuni yake. Ukiondoa matatizo wayapatayo binadamu kwa sababu ya mambo kama mafuriko, nzige, kiangazi, nk, matatizo yao mengi hutokana na ubinafsi”
”Swali ambalo twalisikia mara kwa mara; ” Hali yetu ya baadaye itakuwaje? Mtu anayeuliza anafikiri kuwa TANU iliundwa kwa faida yake yeye binafsi. Ni kama kwamba TANU ilipoundwa ilimwahidi kwamba ikiwa atakubali kuwa mwanachama, au kiongozi, basi, TANU itamfanyia yeye jambo fulani kama tuzo! Anasahau kabisa, kuwa TANU inajishughulisha na haja za jumuiya kwa ujumla.
Lakini, kwa mtu wa aina hiyo, hata kama TANU inatimiza madhumuni yake ya Jumuia, ataona kuwa ni umoja ambao hauna maana kwa sababu haumtimizii haja zote za nafsi yake! Huu ni ubinafsi. Kama wanachama wa TANU, na hasa viongozi, hawatakiuhukumu chama chetu kwa mahitaji ya jamii yao, bali watakihukumu kwa mahitaji ya nafsi zao wenyewe, chama hakitadumu. Wanachama wa aina hiyo ni ugonjwa katika chama”
Mwl. Nyerere anaendelea; ” Dalili nyingine ya ubinafsi, na ambayo ni ugonjwa mbaya sana, ni fitina. Kanuni moja ya TANU inasema; ”Nitasema kweli daima. Fitina kwangu ni mwiko.” Lakini bado tunao wanachama ambao ni wafitini wakubwa bila kujitambua.” (J.K Nyerere ”Tujisahihishe”,1962).
Hakika, uongozi wa CCM ungefikiria kukichapa tena kitabu hiki cha Mwalimu na kukigawa kwa viongozi na wanachama wake. Ni kitabu ambacho kinapaswa kusomwa pia na kila mzalendo wa nchi hii. Maana, aliyoyaandika Mwalimu Nyerere mwaka 1962 ndio yaanayotokea sasa ndani ya CCM. Hakika Mwalimu alikuwa na uwezo wa kuona mbali.
Source: JamiiForum
Comments