TANZIA - KANALI MSTAAFU SAMWEL ELIEZER MOSHA (P1397)


Kuzaliwa 06 JAN 1944 - Kufariki 01 DEC 2017

Mzee wetu huyu amelitumikia Jeshi la Wananchi la Tanzania katika nafasi mbali mbali mpaka anastaafu Jeshi Tarehe 24 SEP 1983 alikuwa na cheo cha Kanali. Amewahi kuwa 'field engineer' na 'inspector'huko Jeshini, amekuwa mwalimu wa maaskari Chuo cha Jeshi Monduli, amekuwa Mwalimu wa wapigania Uhuru mbali mbali wa Afrika huko Nachingwea Tanzania.

Ni rafiki na Mh. Yoweri Kaguta Museveni (Rais wa Uganda) na alikuwa rafiki na Hayati Samora Machel (Aliyekuwa Rais wa Msumbiji).

Amepigana vita ya Uganda, baada ya vita ya Uganda alikuwa Msaidizi wa Waziri Mkuu wa Tanzania Hayati Edward Moringe Sokoine. Amekuwa pia Mkuu wa Wilaya mbali mbali kipindi cha awamu ya Kwanza ya Hayati
Mwl. Julius Kambarage Nyerere. Amekuwa pia Mkurugenzi kwenye Shirika la Bima la Taifa (NIC) kabla ya kustaafu rasmi kwa mujibu wa sheria.


Kanali Mstaafu Samwel E. Mosha alikuwa ni ndugu (rika moja) na Marehemu Baba Yangu Mzazi Alfred S. Mosha, walikua pamoja Kijijini Marangu Masia, walisoma pamoja mpaka Tabora Boys Sekondari ya miaka yao. Baada ya Tabora Boys ndio walipishana, Samwel akaenda Jeshini na Alfred akaingia Serikalini.

Kanali Mstaafu Samwel E. Mosha alikuwa Baba yangu wa Ubatiozo (God Father) na Baba Mlezi baada ya Baba yangu Mzazi Alfred S. Mosha kufariki dunia Tarehe 02 Sept 1994. Amenilea katika mambo yote kama Mzazi na amekuwa rafiki yangu wa karibu na kushiriki matukio yangu yote ya maisha, amekuwa mshauri wangu mkuu kwenye kazi zangu na familia yangu. Pamoja na mambo mengine alinisimamia kidete kuhakikisha napata mwenza na kufunga pingu za maisha kwa mujibu wa Dini yetu.

Hakika nimempoteza mtu wangu muhimu sana na mshauri wangu mkuu, kama familia ni pengo kubwa sana. Tunamshukuru Mungu kwa kutuletea Mzee wetu na kutusaidia, kutusimamia, kutuongoza na kuhakikisha kila mmoja wetu anasimama mwenyewe katika dunia hii. Tunamshukuru Mungu pia kwa maisha yake yote ya Kijeshi, amenisimulia mengi kuhusu maisha yake ya kikazi na baadhi ya operations alizoshiriki, hakika zimenijengea ujasiri mkubwa sana kutambua umuhimu wa kuwa Mzalendo na kuipenda Nchi yetu na kuwasaidia Viongozi wenye dhamana kutekeleza majukumu yao kwa maslahi ya Taifa letu.

Hakika tunamshukuru sana Mungu kwa kutupatia Mzee wetu huyu. Kama binadamu nina majonzi lakini nikitafakari kiimani natambua kazi yake hapa dunia imekwisha kwa Ushujaa Mkubwa. Deni kubwa lipo kwetu wanae kutimiza kwa vitendo yale yote aliyokuwa anatufundisha na kutuusia hasa tukikumbuka baraka zake kila tukionana. 

"Bwana ametoa, Bwana ametwaa, Jina la Bwana wetu Yesu Kristo Lihimidiwe. Amen" 

Comments

Popular posts from this blog

FAMILIA YANGU ILIPOTEMBELEA KIJIJI CHA WATOTO YATIMA CHA FURAHA MBWENI KINACHOSIMAMIWA NA MASISTA WA KATOLIKI WA SHIRIKA LA KIMISIONARI LA BIKIRA MARIA MAMA WA YATIMA SIKU YA JUMAPILI TAREHE 17 JANUARI 2016

Rest In Peace Son of Africa, Meles Zenawi.