Mtazamo binafsi : Dangote Industries (Tanzania) Ltd.

Leo nimeamua kutoa mtazamo wangu kuhusu uwekezaji unavyofanyika hapa nchini kwetu. Kwasababu uwekezaji ni hoja pana (mtambuka) na yenye kuhitaji utaalamu wa sekta mbali mbali, mimi nitatoa mtazamo wangu binafsi kwa namna nilivyoona mimi, kwa kutumia uwekezaji wa Dangote Industries kule Mtwara.

Kwanza kabisa bila kumung'unya maneno nakubali kabisa kwamba uwekezaji ule ni MUHIMU sana kwa uchumi wetu na watanzania kwa ujumla. Ni suala la msingi na linalohitaji kupongezwa. Pamoja na hayo, kuna changamoto zinazojitokeza kwenye kila shughuli. Kwa uwekezaji huu wa Dangote Industries, mimi nimeona changamoto zifuatazo.

Mwekezaji hakutakiwa kupewa gesi ili yeye atumie kuzalishia moja kwa moja umeme wake, nishati ya mitambo na reli ya kuingiza malighafi kiwandani na kutolea cement baada ya uzalishaji. Hapa namaanisha kwamba hakutakiwa kupewa bomba lake peke yake ili yeye azalishe umeme, nishati ya uzalishaji na uendeshaji wa mitambo, kujenga reli yake mwenyewe kuleta mali ghafi kiwandani na kutengeneza gati yake mwenyewe pale bandarini Mtwara ili kusafirishia cement baada ya uzalishaji. Ila kutokana na umaskini wetu na ukosefu wa mitaji ya kuweka miundombinu ndio tumefika hapa.

Kama tungeweka miundombinu hii sisi wenyewe (kuijenga kama serikali au taasisi zake kama TANESCO, TPA, TPDC, nk. Mwekezaji angeuziwa umeme uliozalishwa na gesi husika (TANESCO), angeuziwa nishati ya gesi maalumu kwa ajili ya kuendeshea mitambo (TPDC), angelipia miundombinu ya reli kupeleka malighafi kiwandani na kutoa cement kupeleka bandarini (TRL) na kwingineko, angekodishwa huduma za gati la bandari iliyoboreshwa (TPA), na gati hiyo wangekodishwa na wahitaji wengine. Hapa utaona pato la kampuni au watoa huduma mmoja mmoja lingeongezeka, washiriki wa kuzalisha cement wangeongezeka na pato la taifa lingekua zaidi kutokana na kodi na huduma nyingine. 

Yote haya ni kwasababu ya kukosa mitaji ya kuwekeza na pia kukosa 'SERA' ya gesi na mafuta ambayo ingetoa mwongozo kwenye yote hayo.

Nimegusia Dangote Industries, lakini hoja hii ni mtambuka na inahusu uwekezaji wowote kwenye sekta yoyote hapa nchini. Ni changamoto ambayo LAZIMA kama taifa linalotaka kukomboa raia wake watoke kwenye lindi la umaskini na kuvuka malengo inatubidi kushirikiana na kukubali pale tunapokosea ili turekebishe na kusonga mbele kwa pamoja kama Taifa.

Kwa habari zaidi BOFYA HAPA

Jumamosi njema..

Comments

Popular posts from this blog

FAMILIA YANGU ILIPOTEMBELEA KIJIJI CHA WATOTO YATIMA CHA FURAHA MBWENI KINACHOSIMAMIWA NA MASISTA WA KATOLIKI WA SHIRIKA LA KIMISIONARI LA BIKIRA MARIA MAMA WA YATIMA SIKU YA JUMAPILI TAREHE 17 JANUARI 2016

Rest In Peace Son of Africa, Meles Zenawi.