Kinyozi Mzee kuliko wote...

Hii inaweza kuwa mara ya 300 kwa Mike Jaffe kwenda kunyoa nywele na ndevu kwa Bw. Anthony Mancinelli na pia kupiga blahblah kidogo. Kwa mujibu wa kitabu cha "Guiness Book of World Records", Anthony ndiye kinyozi mwenye umri mkubwa kuliko vinyozi wote duniani.

Ukienda kwa Anthony huishii kunyoa nywele peke yake bali utajikuta unaongelea hali ya hewa ya siku hiyo, nani kaja na nani kaondoka mjini, nani kafa nani kazaliwa, na mambo mengine mengi kama hayo.

Wateja wa Anthony wanasema mzee huyu ambaye atatizmiza miaka 99 Machi 2 mwaka huu ni sawa na maktaba inayotembea katika jiji la New York huko Marekani. Jamaa alianza kunyoa watu nywele na ndevu akiwa na miaka 12, hii ina maana amepiga kazi ya kinyozi kwa miaka 87. Hii ndio sifa inayomfanya Anthony kuwa kinyozi mzee kuliko wote duniani.

Anthony alimwambia Jaffe, "Nilipoanza kazi hii nilikuwa nalipwa senti 5 kwa kichwa". Jaffe amekuwa akinyoa nywele kwa Anthony kwa miaka 25 sasa. "Baadae bei ikapanda kidogo na kufika senti 25 na senti 15 kama unanyoa na ndevu."

Sasa hivi ukienda kunyoa kwa Anthony unaacha dola 12. Wateja wake wanasema jamaa pamoja na umri wake mkubwa bado vidole vyake vina kasi ya ajabu. Jaffe anasema Anthony pia hujinyoa nywele zake mwenyewe.

Wateja wa Anthony wanasema kinachowarudisha kila mara kwenda kunyoa kwake si umaahiri wa kunyoa pekee bali ni pamoja na 'michapo' aliypnayo mzee huyo. Jamaa ni mcheshi kupindukia na anazo stori nyingi mno za miaka 87 ya kazi yake.

Anthony anasema kitu kilichopelekea kufanya kazi hii ya kinyozi ni ujira mdogo aliokuwa akipata baba yake, dola 25 za Kimarekani kwa wiki, aliyekuwa anafanya kazi katika mashine ya kusaga. "Baba yangu alipata ujira mdogo na alikuwa na watoto saba pamoja na mke, pesa ile haikutosha kwa hivyo ikanibidi nianze kufanya kazi nikiwa mdogo ili kumsaidia baba yangu kutunza familia, japo mchango wangu ulikuwa mdogo lakini haikuwa sawa na kukaa bure." Anasema Anthony.

Lakini cha ajabu ni kwamba jinsi siku zilivyozidi kusonga, Anthony akajikuta akiipenda kazi ya kinyozi kuliko ujira aliokuwa akiupata na hivyoo kuamua kuifanya kazi hiyo kuwa kazi yake ya kudumu.

Joe Annunziata, mwenye miaka 69 alifundishwa kunyoa na Anthony, anasema, "Anthony ni zaidi ya mwalimu wangu, ni baba yangu, ni mwongozo wangu. Mzee huyu hunyoa nywele zake yeye mwenyewe, hicho ni kipaji toka kwa Mungu."

Joe anasema siri ya Anthony kufikia umri huu akiwa na nguvu zake na bado akiwa anafanya kazi yake kwa ustadi mkubwa, tena akiwa amesimama wakati wote, ni kutovuta sigara na kutogusa kileo cha aina yeyote.

Nimeona nilete habari hii kwako mwanakijiji ili uone ni jinsi gani ukiweka mapenzi katika kazi yako, hata kama ni ya kufagia barabara, watu watakuheshimu na kukupenda wakati wote. Haya, kila mtu afunge ndoa na kazi yake hadi pale kifo kitakapowatenganisha. 


HABARI NA PICHA KWA HISANI YA MWANAKIJIJI

Comments

Popular posts from this blog

FAMILIA YANGU ILIPOTEMBELEA KIJIJI CHA WATOTO YATIMA CHA FURAHA MBWENI KINACHOSIMAMIWA NA MASISTA WA KATOLIKI WA SHIRIKA LA KIMISIONARI LA BIKIRA MARIA MAMA WA YATIMA SIKU YA JUMAPILI TAREHE 17 JANUARI 2016

Rest In Peace Son of Africa, Meles Zenawi.