Unatafuta ndoa safi asilimia 100? Haipo...

Unatafuta ndoa safi asilimia 100? HaipoDISMAS, LYASSA
HIVI karibuni nilitembelea mikoa ya Arusha, baadaye Dodoma ambapo pamoja na mambo mengine nilikutana na baadhi ya watu na kuzungumza kuhusu mambo tofauti yakiwemo ya ndoa.

Karibu watu wengi niliokutana nao walizungumzia kero katika ndoa huku baadhi yao wakiomba kujua mbinu za kuachana kutokana na kile walichosema kwamba ndoa zimekuwa ni za shida, badala ya faraja waliyoitarajia wakati wanaingia.

�Kaka Lyassa, mimi ni muumini wako, nimekuwa nikisoma sana vitabu na makala ambazo umekuwa ukiandika kwenye magazeti, niliposikia unakuja, nikaona nije nikuone,� alisema mama mmoja ambaye aliomba uandikwe mkasa tu, si jina lake.
�Nisaidie la kufanya ili niachane na mume wangu maana sioni faida ya kuwa naye.�
Swali:Ulitarajia faida gani wakati unaingia kwenye ndoa?
Jibu: Nipate mtu ambaye naweza kusaidiana naye katika maisha,sasa amekuwa ni kero, mambo mengi anajifanyia, kwa mfano sina kazi, yeye ameajiriwa na pia ana biashara, sijui hata huo mshahara wala chochote kuhusu biashara yake, niko tu nyumbani, maisha yangu siyaelewi yanakoelekea.

Swali: Kwa hiyo kuachana ni tiba?
Jibu:Eeeh, bora nijue moja kwamba sina mtu.
Kuna watu wengi ambao matarajio yao kwenye ndoa yamekwenda tofauti. Tafiti zinaonyesha kuwa hali imekuwa mbaya zaidi siku hizi, idadi ya ndoa inaongezeka.
Huenda wewe ukawa ni mojawapo wa waathirika wa matarajio ya ndoa, ulitarajia mazuri, sasa mambo unaona yanakwenda mrama. Fahamu kuwa wewe si mtu wa kwanza.

Tafiti zinaonyesha kuwa asilimia kubwa ya ndoa hazina amani au matarajio yaliyokusudiwa. Kwa mujibu wa utafiti wa hivi karibuni wa chuo kikuu cha Loveology kilichoko eneo la West Hollywood, California, Marekani hakuna ndoa ambayo haina mikwaruzo.

Tofauti iliyoko ni akili za watu waliomo kwenye ndoa, kwamba wengine wanapokuwa na mikwaruzo wanaimaliza mara moja wakati wengine wanaikuza.

Mtafiti maarufu katika masuala ya uhusiano Dk D.Ava, ambaye ni kati ya wakufunzi wa uhusiano anasisitiza kuwa jambo la msingi kwa wanandoa ni kufahamu kuwa mikwaruzo ipo na kinachohitajika ni kwa wanandoa wenyewe kuwa na kawaida ya kukaa pamoja kuondoa tofauti zao.

Aidha utafiti mwingine wa chuo kikuu cha Curtin cha Australia, unaeleza kuwa siri ya wanandoa kuwa na maisha bora, kwanza kujuana kwa kina kabla ya kuanza uhusiano.

Tofauti na ilivyokuwa miaka mingi ya nyuma kwamba watu walikuwa wakijuana kabla ya kuanzisha uhusiano, siku hizi wengi wanakurupuka, na hicho ndicho kinachosababisha ndoa nyingi kuvunjika.

Inasikitisha sana kuona watu waliooana tena wengine kwa harusi za kifahari sana, ndoa zao hazina matunda wala kudumu. Kiapo kile walichokula pale mbele ya Watumishi wa Mungu kwamba tutapendana katika raha na shida kinakuwa batili, leo wala hakikumbukwi tena na badala yake kunatokea vitu vinavyoitwa nyumba ndogo na kubwa.

Kwa Wakristo ambao kimsingi kwao hakuna talaka, baadhi ya wanaume wamekuwa wakihama nyumbani na kuhamia nyumba ndogo au wanafanya siri na wengine wanalala pamoja hakuna tendo la ndoa wala kusemezana. Wengine tendo la ndoa wanapata baada ya kutumia nguvu, maana mwenzake hana hamu naye hata kidogo.

Matajiri, wenye vyeo, wasomi n.k nyumba zao zinatisha. Wengi wao wanaigiza tu kuwa wanapendana lakini hakuna ndoa. Sasa tufanyeje ili kuziponya familia hizi zinazosambaratika.

Inawezekana wewe au mimi ni mmoja wa wenye tatizo hili tufanyeje? Kuna baba mmoja ambaye ameoa lakini akawa ana msichana amempangishia na kumhudumia kwa kila kitu, kanisani ni mzee wa usharika kwa sababu ni tajiri, je wewe kama mwenye kuona hali hii unafanya nini?

Ni watu wangapi wanaimba kwaya leo wanafanya huduma mbalimbali kanisani na hata misikitini lakini nyumbani hakukaliki? Tunawasaidiaje watu wa aina hii au tunaishia kusema chini-chini tu basi? Tafakari chukua hatua.

MUHIMU KUZINGATIA:
*Ni muhimu kwa wanandoa kuepuka mazoea, yaani wawe wabunifu, kwa mfano wanaweza wakawa wanapeana zawadi za kushtukiza, au wanaandaliana safari za kushtukiza, hii inamfanya mwenzi wako aone kwamba unamkumbuka.

*Ni muhimu kuwa muwazi. *Mme/mke amsaidie mwenzake kutimiza malengo yake *Utayari wa kusamehe ni jambo jingine muhimu katika kuimarisha ndoa

*Usikumbushie makosa yaliyopita, lakini zaidi ya yote ukikosea kubali na kuwa tayari kuomba msamaha. *Usilale kabla hujamaliza kulizungumza tatizo au kero inayowasumbua kiasi cha kufanya msielewane.

*Kama kuna umuhimu, wa kupinga hoja ya mwenzako, basi fanya hivyo kwa upendo. *Ndugu yangu mmeoana kwa maana kwamba mnapendana, ni vizuri mshirikishe mwenzake mipangilio yako ya kila siku.

Zaidi ya yote jitahidi kutokasirika au kuendekeza tabia za kununa-nuna, kuna tatizo lizungumzwe yaishe.

Ambacho nataka kifahamike katika makala haya ni kwamba matatizo ni sehemu ya maisha, ndoa kama ndoa ni sehemu ya maisha, elewa kuwa utakuwa na mikwaruzo ya hapa na pale, cha msingi ni kujua namna ya kumaliza kasoro hizo, hatimaye muweze kwenda sawa.

Habari kwa hisani ya :-
Dismas Lyassa, mtaalam wa uhusiano aliyesajiliwa na Serikali (Social Welfare Counselor), simu 0653777700

Comments

Popular posts from this blog

FAMILIA YANGU ILIPOTEMBELEA KIJIJI CHA WATOTO YATIMA CHA FURAHA MBWENI KINACHOSIMAMIWA NA MASISTA WA KATOLIKI WA SHIRIKA LA KIMISIONARI LA BIKIRA MARIA MAMA WA YATIMA SIKU YA JUMAPILI TAREHE 17 JANUARI 2016

Rest In Peace Son of Africa, Meles Zenawi.