Mtoto aadhibiwa kwa kunin'ginizwa mtini kichwa chini miguu juu!


Dickson Mjarifu, mtoto wa miaka minane tu,  mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Dukamba, amepewa adhabu ya kuning’inizwa mtini miguu juu kichwa chini angali amefungwa miguu na mikono yake.

Mtoto huyo mkazi wa kijiji na kata ya Kharumwa wilayani Geita alipewa adhabu hiyo kwa karibu wiki moja na mama yake wa kufikia, Dafroza Masilu (25) kwa kushirikiana na baba yake mzazi, Hezron Mjarifu (35) na kuonywa kuwa angethubutu kusema lolote kuhusu adhabu hiyo, basi angeuawa.


Akisimulia kisa hicho mwanzoni mwa wiki hii katika mahojiano maalumu na gazeti la Serikali la HabariLeo, mwalimu wa darasa analosoma mwanafunzi huyo, Agnes Boniphace, alidai kuwa Alhamisi iliyopita muda wa Asubuhi, wanafunzi wenzie Dickson walitoa taarifa shuleni kuhusu mateso aliyokuwa akipata mwenzao. Kwa mujibu wa Mwalimu Agnes, ambaye sasa anaishi na Dickson, wanafunzi hao walipokuwa wakipita njiani karibu na nyumba anayoishi mtoto huyo, Dickson aliwaita kuwaomba msaada. Wanafunzi hao waliposogea karibu na nyumba hiyo, walimkuta mwenzao amening’inia mtini huku akiomba wasaidie kumnasua kutoka katika mti huo.


“Baada ya kuwaita, wenzake walikwenda na kumwona, wakakimbia hadi shuleni na kutoa taarifa kwa Mwalimu Mkuu, ambaye alituchukua sisi baadhi ya walimu na wanafunzi hao na kwenda kwenye eneo la tukio..." “Tulimkuta Dickson ananing’inia huku amefungwa kamba mikono yote na miguu huku kichwa kikielekezwa chini mfano wa popo..." “Tulipoona hali hiyo, ilitulazimu kutoa taarifa kwa uongozi wa Kijiji ambapo Ofisa Mtendaji wa Kijiji alifika na kushuhudia, tukamfungua akateremshwa na kwenda naye shuleni akatusimulia kila kitu, yakiwamo mateso ambayo amekuwa akifanyiwa na mama huyo wa kambo,’’ alidai Mwl. Agnes.


Walipofika shuleni, walimvua mtoto huyo nguo na kushuhudia makovu sehemu mbalimbali za mwili na hasa mgongoni, makalioni na kifuani, huku akionesha alama za fimbo.  Kutokana na hali ya makovu na alama za fimbo, uongozi wa Shule ulimwita mama huyo na kumhoji juu ya hali ya mtoto huyo.


“Cha ajabu, mama alipofika na kuhojiwa, alisema anayehusika na kipigo cha mtoto huyo ni baba yake mzazi, Hezron Mjarifu, ambaye ni mkulima katika kijiji hicho..." “Tuliamua kuwaita polisi ambao walimkamata mtuhumiwa na kumpeleka kituoni na kumpatia mtoto fomu namba tatu ya matibabu,’’ alifafanua.


Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Kharumwa, Dk. Leonard Mugema, aliyempa matibabu mtoto huyo alisema baada ya uchunguzi wa kina, alibaini mambo mengi yaliyosababishwa na kipigo hicho.  Dk. Mugema alisema walibaini majeraha ya ndani yaliyosababisha damu kuvilia mwilini.


“Hali ya mtoto si nzuri ana makovu mwili mzima akikuvulia nguo kama una roho nyepesi unaweza kumkimbia bila kumpa matibabu ... lakini nashukuru manesi wangu wamejitahidi kumsafisha vidonda vizuri..." “Tulitaka tumlaze, lakini yeye akaomba akae kwa mwalimu wake wa darasa ambaye amekuwa akimleta asubuhi na jioni hapa hospitalini kwa matibabu,” alisema Dk. Mugema.


Dk. Mugema aliongeza kuwa baada ya kumfanyia vipimo vya kina mtoto huyo, walibaini anakabiliwa pia na utapiamlo uliosababishwa na kukosa chakula mara kwa mara.


Akizungumza na gazeti hili, Dickson alidai amekuwa akipigwa kwa mwezi na wiki tatu kila siku na mama yake alimwekea ‘dozi’ ya kuchapwa viboko kila siku asubuhi na jioni.  Alidai pia mara nyingi amekuwa akinyimwa chakula na kufanyishwa kazi nyingi na ngumu, ikiwa ni pamoja na kusomba maji kutoka kisimani na kwenda kusenya kuni porini. Akabainisha kwamba alionywa na mama yake huyo kwamba endapo atatoa siri atauawa, hali iliyosababisha akae kimya siku zote hizo, hadi siku hiyo alipoomba msaada kwa wanafunzi wenzake. Alidai kuwa aliamua kuomba msaada, kwa kuwa mama huyo hakuwapo, kwani alikwenda shambani na kumwacha akining’inia mtini.


from: http://www.wavuti.com/habari.html#ixzz1IB7V32Z7

Comments

Popular posts from this blog

FAMILIA YANGU ILIPOTEMBELEA KIJIJI CHA WATOTO YATIMA CHA FURAHA MBWENI KINACHOSIMAMIWA NA MASISTA WA KATOLIKI WA SHIRIKA LA KIMISIONARI LA BIKIRA MARIA MAMA WA YATIMA SIKU YA JUMAPILI TAREHE 17 JANUARI 2016

Rest In Peace Son of Africa, Meles Zenawi.